6 Juni 2024 - 17:03
Katibu Mkuu wa UN: Lengo la kudhibiti ongezeko la joto duniani 'linaning’inia'

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametahadharisha kuhusu hatari ya wazi ya uwezekano wa kutokea ongezeko la joto juu ya nyuzijoto 1.5 za selsiasi linaloukabili ulimwengu ikiwa uzalishaji wa hewa chafuzi utaendelea kwa viwango vya sasa.

Katika Hotuba Maalumu Kuhusu Hatua Dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi, ambayo ameipa jina la "Wakati wa Ukweli", Guterres amelitumia jukwaa hilo kuueleza ulimwengu ukweli kwamba utafiti wa kitaalamu unaonesha kuwa ni tani bilioni 200 tu za hewa ukaa ambazo dunia inaweza kuzihimili kabla ya kuvuka nyuzijoto 1.5 za Selsiasi juu ya viwango vya kabla ya viwanda jambo ambalo ni hatari kubwa kwa ulimwengu.

Itakumbukwa kuwa chini ya Mkataba wa Paris mnamo mwaka 2015, nchi zilikubaliana kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa hewa chafuzi ili kuwezesha ongezeko la muda mrefu la wastani wa joto la uso wa dunia kuwekwa chini ya nyuzijoto 2 za selsiasi juu ya viwango vya kabla ya kuanza kwa viwanda na kuendeleza juhudi za kulipunguza joto hadi nyuzijoto 1.5 za selsiasi kisha kuhakikisha halizidi hapo.Lakini kiongozi huyu wa Umoja wa Mataifa ameyakumbusha mataifa kwamba kwa kasi ya sasa ya uzalishaji hewa chafuzi kwa kiasi cha tani bilioni 40 kwa mwaka ni wazi kuwa uwezo wa dunia kuendelea kudhibiti joto lisipande utaisha mapema. Katika hotuba yake hiyo Guterres amesisitiza kuwa hakuna nchi inayoweza peke yake kutatua janga la tabianchi akisema, “huu ni wakati wa kila mtu kushiriki. Umoja wa Mataifa unajitolea kufanya kazi ili kujenga uaminifu, kutafuta ufumbuzi, na kuhamasisha ushirikiano ambao ulimwengu wetu unahitaji sana.” Akiashiria maafa yanayoendelea kuikumba dunia kutokana na mabadiliko ya tabianchi, Katibu Mkuu wa UN amesema, "tayari mwaka huu, wimbi la joto kali limeioka Asia na halijoto iliyorekodiwa ikinyausha mazao, kufunga maskuli na kuua watu. Miji kutoka New Delhi, hadi Bamako, hadi Mexico City inaungua. Hapa Marekani, dhoruba kali zimeharibu jamii na maisha. Tumeona majanga ya ukame yakitangazwa kote kusini mwa Afrika; mvua kubwa zikifurika Rasi ya Uarabuni, Afrika Mashariki na Brazili; na upaukaji mkubwa wa matumbawe ulimwenguni unaosababishwa na joto lisilo la bahari, zaidi ya walivyotabiri wanasayansi".../

342/